Viongozi wa maeneo husika watashauriana ili kuamua jinsi ya kufanya sakramenti ipatikane kwa waumini angalau mara moja kwa mwezi
Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili wa Kanisa La Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho wametuma barua ifuatayo Machi 12, 2020, kwa waumini wa Kanisa ulimwenguni kote.
Wapendwa akina Kaka na akina Dada,
Kama ilivyoahidiwa katika barua yetu ya Machi 11, 2020, tunaendelea kufuatilia hali ya mabadiliko kuhusiana na COVID-19 kote ulimwenguni. Tumezingatia ushauri wa viongozi wa Kanisa wa maeneo husika, viongozi wa serikali na wataalamu wa afya na tumetafuta mwongozo wa Bwana katika masuala haya. Sasa tunatoa maelekezo mapya yafuatayo.
Kuanzia sasa, mikutano yote ya umma ya waumini wa Kanisa inasitishwa kwa muda ulimwenguni kote hadi taarifa ya baadaye. Hii inajumuisha:
- Mikutano ya vigingi, mikutano ya uongozi na mikutano mingine mikubwa
- Huduma zote za umma za kuabudu, ikiwa ni pamoja na mikutano ya sakramenti
- Shughuli za tawi, kata na kigingi
Pale inapowezekana, tafadhalini fanyeni mikutano yoyote ya muhimu ya uongozi kupitia teknolojia. Maswali mahususi yanaweza kupelekwa kwa viongozi wa ukuhani wa maeneo husika. Maelekezo zaidi kuhusiana na masuala mengine yatatolewa.
Maaskofu wanapaswa kushauriana na rais wao wa kigingi ili kuamua jinsi ya kufanya sakramenti ipatikane kwa waumini angalau mara moja kwa mwezi.
Tunawahimiza waumini katika juhudi zao za kuhudumu kumjali kila mmoja. Tunapaswa kufuata mfano wa Mwokozi wa kubariki na kuinua wengine.
Tunatoa ushahidi wetu wa upendo wa Mwokozi wakati wa kipindi hiki cha wasiwasi. Yeye atawabariki mpate shangwe pale mnapojitahidi kadiri ya uwezo wenu kuishi injili ya Yesu Kristo katika kila hali.
Wenu waaminifu,
Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili